Sasa ni kati ya Chama cha Tiba Asili (ATME) na TDFA.
ATME kinadai hayana madhara wagonjwa wake wameyatumia kwa zaidi ya miaka
20.
Dar es Salaam. Mratibu wa Chama
cha Watabibu wa Dawa za Asili Tanzania (ATME), Boniventure Mwalongo
amesema taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TDFA) kuhusu matumizi ya mafuta ya ubuyu zinaweza kuleta madhara kwa
jamii kwa sababu watu wengi wamekuwa wakiyatumia.
Akitolea mfano watumiaji wakubwa wa mafuta hayo,
Mwalongo alisema, wenye magonjwa kama ya moyo na wanaoishi na Virusi vya
Ukimwi wamekuwa wakiyatumia mafuta hayo kwa muda mrefu na kudai
yamewasaidia.
Mwalongo ameyasema hayo jana baada ya hivi
karibuni kuibuka utata kuhusu ubora na usalama wa mafuta hayo na kudai
kuwa wao kama ATME walianza kuyatumia kama dawa kwa wateja wao siku
nyingi na hawajawahi kupata malalamiko yoyote na kuwahakikishia
watumiaji kuwa hayana madhara.
“Yametumika kwa zaidi ya miaka 20 na sisi tunazo
kumbukumbu za wagonjwa tuliowapa mafuta hayo kama dawa na hatujawahi
kupata ripoti yoyote ya madhara kwa wale waliotumia,” alisema
Mwalongo. TFDA ilitoa taarifa kwamba mafuta hayo hayafai kwa matumizi
ya binadamu kwa sababu yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina
ya cyclopropenoic fatty acids.
Katika taarifa ya TFDA iliyotolewa juma
lililopita ilisema athari zinazoweza kutokea kutokana na matumizi ya
mafuta hayo ni pamoja na kuathiri vimeng’enyo vinavyosaidia katika
uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini.
Pia ilisema ili yaweze kukidhi vigezo vya ubora
na usalama ni lazima yafanyiwe usafishaji wakati wa usindikaji na kwamba
kwa sasa nchini hakuna aina ya usindikaji unaofanyika wenye uwezo wa
kuondoa tindikali hiyo ya cyclopropenoic fatty acids katika mafuta ya
mbegu za ubuyu.
Hata hivyo Mwalongo alikemea usambazaji holela wa
mafuta hayo hasa baada ya kubainika kuwa yanatibu maradhi mbalimbali
ambapo baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakiyasambaza wakati siyo
wataalamu wa tiba asili.
Mratibu huyo alizishauri mamlaka zinazohusika na
suala zima la afya ya binadamu nchini kutoa majibu yatakayosaidia
kuondoa mgawanyiko uliopo sasa kutokana na mafuta hayo badala ya kutoa
taarifa za kutisha.
Hata hivyo alipoulizwa Kaimu Mkurugenzi wa
Kitengo cha Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paul
Mhame, alisema hawana taarifa zozote kama kuna tafiti zimefanyika
kuhusiana na matumizi ya mafuta hayo.