Kampuni ya Bia ya East African Breweries Limited (EABL) imeahidi kutoa Dola za Kimarekani 400,000 kwa ajili ya kuendesha Mashindano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na ya Kati, CHALENJI CUP 2012, yatakayochezwa huko Kampala, Uganda kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, Fedha hizo ni za udhamini ambao utalipia gharama za usafiri, malazi na Zawadi kwa Washindi zikiwa ni Dola 30,000 kwa Bingwa, Dola 20,000 kwa Mshindi wa Pili na Dola 10,000 kwa Timu ya Tatu.
Wakati huo huo, CECAFA imekubaliana na Waongoza Kampeni dhidi ya Malaria, United Against Malaria (UAM), kushirikiana na kuongeza nguvu kukabiliana na Ugonjwa huo wakati wa michuano ya CHALENJI CUP 2012.
Akizungumzia makubaliano hayo, Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga, ambae aliisifia UAM katika kampeni yake ya kujaribu kuuondoa Ugonjwa wa Malaria ifikapo 2015 kama ilivyopangwa na Umoja wa Mataifa, amesema: “Mafanikio yetu kwenye Soka yanaathiriwa sana na Malaria hasa kwetu, Familia zetu na Rafiki zetu. Lazima tuelimishe Jamii hatari za Malaria.”
Kwenye CHALENJI CUP 2012, Sudan ya Kusini, Mwanachama mpya wa CECAFA, wanatarajiwa kushiriki kwa mara ya kwanza na hii ni mara ya pili kwa Nchi hiyo mpya kucheza Mashindano ya CECAFA, mara ya kwanza ilikuwa kwenye Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki ya Kati, KAGAME CUP, yaliyochezwa Dar es Salaam Mwezi Julai na Nchi hiyo kuwakilishwa na Wau El Saalam ambapo Yanga walitwaa Ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
KWA MATANGAZO MBALIMBALI KUHUSU BIASHARA YAKO USISITE KUJITANGAA KUPITIA (KIKWATOJR.BLOGSPOT.COM) WASALIANA NASI KWA SIMU NAMBA +255718991013.+25575433520
No comments:
Post a Comment